WINGU
limegubika sakata la kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven
Ulimboka siku moja baada ya kurejea nchini, huku watu wake wa karibu
akiwamo baba mzazi, wakigoma kusema chochote kumhusu.Dk Ulimboka
alirejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa ajili
ya matibabu kwa takriban mwezi mmoja na nusu, baada ya kutekwa, kuteswa
na kutupwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo na Jiji la Dar es Salaam
usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.
Ingawa
wakati wa ugonjwa wake baadhi ya watu wake wa karibu walikuwa wakitoa
maelezo mbalimbali, jana wote waligoma kusema chochote, huku jitihada za
gazeti hili kumpata nyumbani kwake zikigonga mwamba.Baba mzazi wa Dk
Ulimboka, Stephen Mwaitenda aliweka wazi kuwa ni vigumu kumwona daktari
huyo jana.Takriban watu wote waliofika nyumbani kwa Mzee Mwaitenda jana
kumjulia hali Dk Ulimboka waliambiwa kuwa hayupo nyumbani.
Mwaitenda
alilieleza gazeti hili kuwa ana furaha kuwa mtoto wake alirejea nchini
salama licha ya kupelekwa Afrika Kusini akiwa taabani kutokana na
kipigo.
Alipotakiwa
kueleza juu ya kile kilichompata, mtoto wake huyo alisema: "Mungu na
Steven mwenyewe (Dk Ulimboka) ndio wanaojua kilichotokea."Aliongeza:
“Kweli nimefurahi kwamba mwanangu amerudi, lakini siwezi kuelezea nini
kilimtokea alipotekwa," alisema Mwaitenda.Alisema Dk Ulimboka hayupo
nyumbani na hajui kwamba angerudi wakati gani. "Hata kama angekuwapo, ni
vigumu kumwona," alisema.
Kauli ya Katibu wa Madaktari
Katibu
wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema madaktari walikuwa
hawajaamua nini kingefuata baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini.Alisema
hata hivyo, daktari huyo anahitaji muda wa kupumzika kwanza na familia
yake.“Aliporudi jana (juzi) alitumia muda wake kukaa na familia yake,
mpaka sasa hatujajua hatua inayofuata. Dk Ulimboka atazungumza wakati
mwafaka ukifika,” alisema Dk Chitage.
Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi hakutaka kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa alikuwa mkutanoni.
Dk
Mkopi alitoa kauli hiyo baada ya daktari aliyemtibu Dk Ulimboka wakati
wa tukio la kutekwa, Profesa Joseph Kahamba akiwa amesema yeye (Mkopi)
ndiye angesaidia kupatikana kwa Dk Ulimboka ili azungumze na waandishi
wa habari.
Dk Chitage alipoulizwa nini kinaendelea baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini alijibu, "Hakuna kinachoendelea."
Aliendelea, "Leo hakuna kitu, tumepumzika na hata yeye tumemwacha apumzike na familia yake," alisema Dk Chitage.
Alisema
Jumuiya hiyo na familia yake wanaandaa mazingira yatakayowezesha Dk
Ulimboka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari.
"Kuhusu
hatua zitakazofuata tutaandaa utaratibu na tutawaarifu, juu ya hatua
zipi tutachukua ikiwamo hili linaloumiza vichwa vya wengi la mazingira
ya kutekwa kwake," alisema Dk Chitage.
Katibu
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rodrick Kabangila alipoulizwa
kuhusu suala hilo alisema yuko safarini na hajui kinachoendelea.
"Nipo Mwanza, nimesafiri na sijui kinachoendelea," alisema.
Alisema
MAT itakutana kujadili suala hilo wakati wowote na kwamba utaratibu
utaandaliwa kwa Dk Ulimboka kuzungumza na vyombo vya habari.
"Unajua
sisi tuliomba kibali cha kuandamana kushinikiza Serikali kuunda tume
huru kuchunguza tukio hilo na kuwabaini waliohusika tukakataliwa. Lakini
sasa yeye amerudi na anawajua waliomdhuru. Tutaandaa utaratibu,
atazungumza nanyi ili watu wote wajue," alisema Dk Kabangila.
Mkurugenzi
wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya,
alisema hakuwa na mawasiliano yoyote na Dk Ulimboka wala hajui
kinachoendelea baada ya kuachana naye juzi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Nyerere.
Polisi wazungumza
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza
kupitia msaidizi wake, alisema kuwa suala la Dk Ulimboka limefungwa na
hawezi kulizungumzia tena kwa kuwa lipo mahakamani.
"Kamanda
alikwishasema kuwa suala hilo lipo mahakamani hivyo hawezi
kulizungumzia," alisema msaidizi huyo.Alipoulizwa iwapo polisi ilikubali
maombi ya madaktari kutaka tume hiyo ivunjwe na iundwe nyingine huru
alijibu, "Tume inaendelea na kazi.""Tume inafanya kazi yake na polisi
pia wapo katika kazi zao," alisema na kukata simu.
Wanasiasa watoa wito
NCCR-Mageuzi,
CUF na Democratic (DP) vimemtaka Dk Ulimboka kuwataja watu waliomteka
na kumpiga.Wito huo ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Katibu Mkuu wa
NCCR-, Samwel Ruhuza, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro na
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila.“Atumie roho yake na
dhamira yake kuwataja watu waliomfanyia unyama ule ili jamii ijue na
pengine ndio utakuwa mwisho wa watu kufanyiwa vitu vya aina hii,”
alisema Ruhuza.
Ruhuza
alisema kuwa kiongozi huyo wa madaktari amerejea huku akiwa na afya
njema, lakini bado ana deni kwa watu wasiopenda vitendo vya
unyanyasaji.“Ndiyo maana nikasema azungumze jambo hili kutoka ndani ya
moyo wake,” alisema Ruhuza.Mtikila alisema licha ya kwamba Dk Ulimboka
anatakiwa kuwataja waliomfanyia vitendo hivyo, yaliyomkuta yanatakiwa
kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki za
Binadamu.“Nimeshazungumza na mtu mmoja kutoka mjini London, Uingereza
amesema kuwa jambo hilo linawezekana,” alisema Mtikila.Alifafanua
kwamba, atafanya kila njia ili akutane na Dk Ulimboka na kumshawishi
akafungue kesi katika mahakama hiyo ili liwe fundisho kwa wanaopenda
kuwanyanyasa Watanzania wanaodai haki zao.
“Nitafanya
kila njia ili nionane na Ulimboka, hili jambo ni lazima lifike katika
mahakama ya kimataifa ya haki za binadamu…, pia anatakiwa kuwataja
waliomfanyia unyama huu,” alisema Mtikila.
Kwa
upande wake, Mtatiro alisema kuwa Ulimboka anatakiwa kukutana na vyombo
vya habari na kueleza mambo yote ili kufichua yaliyokuwa yakifichwa na
vyombo vya usalama.
“Ukweli
utamweka huru na utawaweka huru watu wengi ambao wanaweza kufanyiwa
unyama siku zijazo. Ikiwezekana afungue kesi ili haki itendeke,” alisema
Mtatiro na kuongeza:“Ulimboka anatakiwa kufahamu kwamba Watanzania
hawakukubaliana na mateso aliyopewa, unyama aliofanyiwa unalaaniwa na
kila mtu,” alisema Mtatiro.
Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe, Aidan Mhando, Joseph Zablon, Geofrey Nyang’oro, Boniface Meena na Leon Bahati.