Salim Kikeke Ndiye mtangazaji wa kipindi hiki
BBC Idhaa ya Kiswahili kuzindua Dira ya Dunia kupitia Star TV nchini Tanzania
23 August 2012.
Katika mpango mkubwa wa kutanua wigo wake wa wasikilizaji na watazamaji
barani Afrika, BBC imetangaza kuzindua kipindi chake cha kwanza cha
habari za dunia kwa lugha ya Kiswahili kiitwacho Dira ya Dunia. Kuanzia Jumatatu Agosti 27, kituo shirika cha BBC Idhaa ya Dunia nchini Tanzania, Star TV, kitarusha kipindi cha Dira ya Dunia
cha BBC Idhaa ya Kiswahili. Matangazo hayo ni ya dakika 30 yakiwapa
watazamaji fursa ya kupata habari motomoto za dunia na uchambuzi
yakinifu kutoka katika shirika hilo la utangazaji la kimataifa
ulimwenguni.
Kipindi
hicho ambacho kitakuwa kikirushwa kila Jumatatu hadi Ijumaa kitatoa
chachu katika matangazo ya Star TV kwa kuwaletea watazamaji habari za
kiwango cha hali ya juu kutoka katika kitovu cha habari za dunia cha
BBC- Global News. Dira ya Dunia pia itawaletea watazamaji taswira na
uchambuzi yakinifu kutoka kwa waandishi wa habari waliotapakaa katika
nchi 48 barani Afrika, na hivyo kuleta picha halisi ya bara zima kwa
watazamaji wanaozungumza Kiswahili.
Kipindi cha radio cha Dira ya Dunia
ni kipindi maarufu sana kwa mamilioni ya wasikilizaji katika eneo la
Afrika Mashariki na Kati na hata wasikilizaji wanaoishi nje ya eneo
hilo. Kwa kuzindua kipindi cha TV chenye jina kama hilo, BBC ina
imarisha zaidi matangazo yake hasa kwa kutumia waandishi wake wa habari
waliobobea – watangazaji Salim Kikeke na Charles Hilary, mhariri Mariam
Omar pamoja na waandishi waliopo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo, Kenya, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania,
Uganda na Uingereza.
Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Ali Saleh anasema: “Uzinduzi wa Dira ya Dunia
kupitia TV, ni kwenda na mabadiliko makubwa tunayoyashuhudia ya jinsi
watu wanavyofuatilia habari barani Afrika, na pia mahitaji wa mashabiki
wa BBC Ihdaa ya Kiswahili. Tunavyoarifu na kuchambua habari za eneo letu
na hata duniani, iwe siasa, uchumi au utamaduni, Dira ya Dunia itatoa
taswira halisi ya Afrika, tofauti na jinsi ambavyo bara hili limekuwa
likiripotiwa kwa miaka mingi. Kipindi chetu kitakuwa kinashirikisha
watazamaji, na pia kuzigatia misingi ya BBC ya muda mrefu ya uhuru,
uhakika na bila upendeleo”
Kinara wa Dira ya Dunia,
Salim Kikeke ameongeza kwa kusema: “Ni heshima kubwa na nafasi ya
kipekee kuwa katika mradi huu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC wa TV.
Tumepitia mengi hadi kufika hapa, na kila sekunde ya safari hiyo ilikuwa
ni ya kuvutia.Ni imani yangu kuwa kipindi hiki kipya cha TV kitavutia
wengi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.”
Uanzishaji
wa Dira ya Dunia katika TV ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya matangazo
yaliyofanyika ndani ya BBC mwaka huu katika bara la Afrika, katika TV
na redio. Uzinduzi huu umekuja muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa
kipindi cha TV kwa lugha ya Kiingereza kwa Afrika, Focus on Africa,
ambacho pia kinarushwa kupitia Star TV. Mwezi Julai, siku chache kabla
ya kuanza kwa michuano ya Olimpiki jijini London, BBC Idhaa ya Ulimwengu
ilizindua kipindi kipya cha redio, Newsday – Kipindi ambacho kimelenga
zaidi wasikilizaji wa redio wa asubuhi barani Afrika.
Mhariri
wa BBC wa eneo la Afrika, Solomon Mugera, naye amesema: “Miongo mingi
ya utangazaji katika lugha mbalimbali barani Afrika, BBC imejenga
uhusiano wa kipekee na wasikilizaji wetu wa redio, kwa kueleza ya Afrika
duniani, na kuipeleka dunia barani Afrika. Kukua kwa njia za utangazaji
za BBC ni ushahidi wa kuwepo kwa mizizi ya muda mrefu na ufahamu wa
bara la Afrika. Tunavyoanza safari hii mpya, kwa kweli tuna hamasa kubwa
hasa kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji yenye hadi kubwa
katika eneo letu.”
Nathan
Lwehabura, Meneja mipango na utafiti wa SMG Ltd, anasema: “ Ni heshima
kubwa kwa Star TV kujumuisha Dira ya Dunia katika vipindi vyake vya kila
siku – tunaamini kipindi hiki kitavutia watu wengi. Kipindi cha BBC cha
Kiingereza kilichozinduliwa hivi karibuni kupitia Star TV, Focus on Africa,
kinazidi kujipatia umaarufu mkubwa, sio tu miongoni mwa watazamaji
wetu, bali pia hata miongoni mwa mashirika mengine kutokana na
kuzingatia fani ya uandishi, utangazaji na ubora wa kipindi. Ni
matumaini yetu kuwa ushirika kati ya BBC na Sahara Media Group
utaimarisha matangazo yetu ya TV hasa tunavyoelekea katika matangazo ya
kisasa ya mfumo wa digital.”
Dira ya Dunia
kutoka Idhaa ya Kiswahili ya BBC itakuwa ikitangazwa Jumatatu hadi
Ijumaa, saa tatu usiku kupitia Star TV nchini Tanzania. Pia matangazo
hayo yatapatikana kupitia wavuti wa BBC Idhaa ya Kiswahili –
bbcswahili.com.
BBC
ilirusha matangazo yake ya kwanza kabisa barani Afrika zaidi ya miaka
80 iliyopita. Idadi kubwa ya wasikilizaji kwa ujumla kupitia redio na TV
inaifanya BBC kuwa shirika kubwa zaidi la kimataifa la utangazaji
barani Afrika.
Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:
BBC Global News Press Office
Kwa wahariri:
BBC Idhaa ya Kiswahili ni
watangazaji wa habari kupitia TV, redio na kwenye mtandao kwa lugha ya
Kiswahili na kwa wasikilizaji na watazamaji wa lugha hiyo. Matangazo ya
redio kwa Kiswahili yanapatikana kupitia vituo vya redio vya FM na pia
kupitia redio washirika nchini Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo, Kenya, Malawi, Mozambique, Rwanda na Uganda. Matangazo pia
yanapatikana kupitia wavuti bbcswahili.com ambapo pia habari mpya kabisa
zinapatikana, makala na uchambuzi kuhusu Afrika Mashariki na pia
duniani kote, kwa maandishi, sauti na video.
BBC Idhaa ya Kiswahili ni sehemu ya BBC Idhaa ya Dunia (BBC World Service), ambao
ni watangazaji wa kimataifa wanaotoa huduma ya matangazo kwa lugha
mbalimbali kupitia redio, TV na kwenye wavuti na pia kupitia vifaa
vitumiavyo visiwaya. Kwa taarifa zaidi tembelea bbcworldservice.com.
BBC ina mashabiki milioni 239 kwa wiki duniani kote katika huduma zake za habari za kimataifa ikiwemo BBC World Service, BBC World News TV na bbc.com/news.