Wednesday, August 15, 2012

AKUTWA AMEFARIKI NDANI YA BASI LA UPENDO MOROGORO


Mwandishi wetu, Morogoro Yetu

Abiria mmoja aliyekuwa akisafiri kwa basi la kampuni ya Upendo lililokuwa likitokea jijini Mbeya kuelekea dar es salaam, amegunduliwa kufariki dunia ghafla, baada ya basi hilo kufika mjini Morogoro.

Mwili wa abiria huyo ambaye tiketi aliyokuwa nayo mfukoni imemtambulisha kama Petro Mrenge Sins, anayedaiwa kuwa mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, umekutwa umelala katika viti vya chini, nyumba ya basi hilo la abiria, ambapo baada ya upekuzi, amekutwa akiwa na mfuko wa nailoni maarufu kama rambo uliokuwa na nguo zake kadhaa, shilingi elfu nne na tiketi ya basi.

Madereva wa basi hilo la Upendo, Marco Paulo na msaidizi wake Juma Abdul, wamedai wamegundua kufariki kwa abiria huyo, baada ya kufika, kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha msamvu mkoani Morogoro, ambapo walitangaza abiria wanaoshuka wafanye hivyo, lakini hakufanya hivyo na kuambiwa abiria huyo alionekana kukosa fahamu, ambapo walitoa taarifa kwa askari waliopo kituoni hapo, na mwili wake kushushwa kituo kikuu cha polisi cha mjini morogoro.

Abiria waliokuwa wakisafiri na mzee huyo aliyepoteza maisha, ambaye kiumri anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 60 hadi 70, tangu majira ya saa 12 afajiri kutokea mbeya, Josephat Mahaulane na Winfrida Andrew, wamedai kufahamiana na mzee huyo tangu jumatatu jioni ambapo alisaidiwa kwa kuchangiwa fedha na wauza matunda wa soko kuu la mjini mbeya na abiria waliokuwa kituo kikuu cha mabasi, baada ya kudai hakuwa na uwezo wa kusafiri.

Aidha wamedai abiria huyo alieleza kutaka kuja mjini Morogoro ambako angeweza kuonana na ndugu, jamaa na marafiki zake, ambao wangemuwezesha kuelekea mkoani tabora.

Mwili wa marehemu huyo ambao pia umekutwa na karatasi ya polisi inayoonesha alihitaji kusaidiwa kufika Morogoro, umepelekwa kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, ukisubiri kutambuliwa na taratibu nyingine za kiuchunguzi.

Habari na Morogoro yetu

0 comments:

Post a Comment