Thursday, September 6, 2012

Makubaliano ya amani yaafikiwa migodini

Wachimba migodi walioshtakiwa kwa mauaji ya wenzao 34
Makubaliano ya amani yanayolenga kusitisha ghasia yameafikiwa kuhusiana na mgogoro wa mishahara ya wachimba migodi unaoendelea nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo duru zinaarifu kuwa makubaliano hayo hayakuhusisha waakilishi wakuu wa wachimba migodi hao.
Hapo awali, mwanaharakati wa kisiasa nchini Afrika Kusini, Julius Malema, alitoa wito wa wachimba migodi kuendelea na mgomo wao hadi matakwa yao yatakapotimizwa na waajiri wao.
Tamko la Malema linakuja wakati mgogoro wa mishahara kati ya wachimba migodi wa Marikana na waajiri wao ukitokota.
Bwana Malema hata hivyo anasema kuwa tamko lake sio uchochezi wa ghasia.
Takriban wachimba migodi, 34 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi tarehe kumi na sita mwezi Agosti.
Wachimba migodi zaidi walioshtakiwa kwa madai ya kusababisha mauaji hayo, wanatarajiwa kuachiliwa baadaye leo.
Vyama kadhaa vya wafanyakazi, vimetia saini makubaliano yatakayowafanya kurejea kazini, kulingana na wamiliki wa migodi hiyo.
Bwana Malema anatarajiwa kuzuru mgodi wa Marikana hii leo, siku moja baada ya wachimba migodi 3,000 kuandamana kuunga mkono wachimba migodi wenzao
Aidha Malema, ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha ANC tawi la vijana, alifukuzwa chamani baada ya kuonekana kutofautiana kwa sera na rais Jacob Zuma.
Bwana Malema awali aliwataka wachimba migodi hao kuendelea kutatiza shughuli za migodi.
Aliambia BBC kuwa '' Watu wametafsiri visivyo wito wangu kwa wachimba migodi kutatiza kabisa shughuli za migodi. Nilicho maanisha ni kwamba waendelee kugoma. Sipendekezi, ghasia wala vurugu wala sitoi wito wa mauaji. Wafanyakazi hawapaswi kukubali kunyanyaswa. Hatutaki dhulma tena, ila ikiwa tu serikali itakubali kuwalipa pesa za kutosha ''
Malema alisema muwa waekezaji wa kigeni wameiba kila kitu nchini Afrika Kusini na akasema kuwa wako tayari kufanya kila hali kurejeshewa kila kilicho chao.
Alisema jibu lililosalia kwa matatizo ya migodini ni kutaifisha migodi.
Siku ya Jumatano, wachimba migodi wa Marikana, walifanya maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mauaji ya wafanyakazi wenzao kuzua hisia kali.
Wachimba migodi hao wanaolipwa kati ya dola miatatu na mianne wanataka nyongeza ya hadi dola miasaba au mianane kwa mwezi.
chanzo: bbcswahili

0 comments:

Post a Comment