*Wakabiliwa na kesi ya kuchochea vurugu
*Kufikishwa mahakamani leo kujibu mashitaka
JESHI la Polisi visiwani Zanzibar, limewakamata viongozi wa Jumuiya ya
Uamsho, akiwemo Sheikh Farid Hadi Ahmed (41), kutokana na kosa la
kuchochea vurugu.
Taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao, zilitolewa na kuthibitishwa na
Kamishna wa Jeshi la Polisi visiwani humo, Mussa Alli Mussa.
Mbali na Sheikh Farid viongozi wengine waliokamatwa ni pamoja na
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Mselem Alli Mselem (52) na Sheikh
Azan Farid Hamad (48).
Wengine ni Sheikh Hassan Bakari Suleiman (29), Ustadh Mussa Juma Issa (33) na Sheikh Suleiman Juma Suleiman.
Kamishna Mussa, alisema viongozi hao wanashikiliwa kwa kosa la kuchoche vurugu, ghasia na kuharibu miundombinu ya barabara.
Kamishina Musa alisema, baada ya viongozi hao kuhojiwa juzi na
kuruhusiwa, lakini jeshi lake limeamua kuwakamata tena viongozi hao
kutokana na uchunguzi wao kubaini viongozi hao walihusika na kuchochea
vurugu visiwani humo.
Kamishina huyo alisema, viongozi hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani
leo kujibu mashitaka yanayowakabili, huku akiwataka wananchi visiwani
humo kuwa watulivu.
“Baada ya kufanya mahojiano na viongozi hawa kwa siku ya juzi na
uchunguzi wetu wa kina, tumebaini viongozi hawa walihusika na kuchochea
vurugu zilizotokea Zanzibar.
“Katika kipindi chote cha mahojiano, tuliweza kutoa haki ya kuwasilikiza kwa kina viongozi hawa.
“Lakini baada ya uchunguzi wetu wa kina tumebaini kuhusika kwa viongozi hawa na matukio ya uvunjifu wa amani hapa Zanzibar.
“Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri katika kulinda usalama wa raia na
mali zao, hasa katika kipindi hiki ambacho Zanzibar imerejea katika hali
ya amani.
“Hivyo tumejipanga vema na wale ambao watajaribu kuvunja amani, tutapambana nao kwa kutumia nguvu.
“Mara baada ya kufanya mahojiano nao viongozi hawa na kujiridhisha kwa
kina kesho (leo) tutawafikisha mahakamani kwa hatua zaidi.
“Jeshi la Polisi tupo imara wakati wote katika kulinda amani na usalama,
hivyo ninatoa wito kwa wananchi kuwa watulivu,” alisema Kamishna Mussa.
Walioua askari watiwa nguvuni
Wakati huo huo jeshi hilo limewatia nguvuni watu sita kwa tuhuma za
kuhusika na tukio la kumuua askari Polisi Koplo Saidi Abdrahamani Juma
(41).
Koplo Saidi, aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Ziwani Mjini
Zanzibar, aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa
ni wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho.
Kamishna Mussa Ali Mussa, alisema watu hao waliokamatwa ni Abdallah Mohamed Said, Joli Ghasul na Bakarin Juma Yussuf.
Alisema watuhumiwa wengine waliokamatwa mkoani Tanga ni Ally Salum Seif,
Abubakari Haji Mbaruk na ndugu yake Mohamed Haji Mbaruk.
“Hawa wengine tumewakamata mkoani Tanga baada ya kuweka mitego yetu ya
kiitelijensia kwa nchi nzima, hivi sasa tumeshawarushisha wapo hapa
Zanzibar, tunaendelea na uchunguzi dhidi yao ambapo wakati wowote kutoka
sasa tunaweza kuwafikisha mahakamani,” alisema Kamishna Mussa.
“Tuelewe kuwa aliyeuliwa ni askari Polisi, ni raia wa Tanzania na ni
muumini wa dini, ni lazima tuhakikishe waliofanya unyama huu wanakamatwa
na kufikishwa mahakamani kama sheria za nchi zinavyotuelekeza,”
alisema.
“Watu hao walitorokea huko na tunaendelea kuwahoji…tunawashukuru
wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliotuwezesha kufanikisha ukamataji
huo,tunavishukuru vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyo katika Shehia
mbalimbali, kwa kuimarisha ulinzi wa maeneo yao katika kipindi chote cha
fujo na vurugu hizo,” alisema Kamishna Mussa.
Oktoba 16, mwaka huu fujo zilizuka visiwani humo baada ya kupotea katika
mazingira ya kutatanisha kwa kiongozi wa jumuiya hiyo, Sheikh Farid
Hadi Ahmed, hali iliyosababisha vurugu.
Sheikh Farid ambaye amekuwa mwiba mkali kwa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ), alionekana saa 2:15 usiku wa juzi katika eneo la
Mazizini, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Watu 51 walikamatwa na Jeshi la Polisi, kutokana na vurugu zilizotekea
visiwani humo, baada ya kuripotiwa kupotea kwa kiongozi huyo.
Via Mtanzania
0 comments:
Post a Comment