WAZIRI
wa zamani wa Fedha, Basil Mramba ameanza kujitetea katika kesi ya
matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia Serikali hasara ya
Sh11.7 bilioni huku akiwataja mashahidi sita akiwamo aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge kuwa mashahidi wake.
Mashahidi
wengine watakaomtetea Mramba katika kesi hiyo, ni Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), Mwakilishi wa Kampuni ya M/S Alex Stewart Government
Business Assayers, Erwine Florence, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali, John Cheyo na Mtaalamu wa Ushauri wa
Masuala ya Kodi, Florian Msigala.
Baada
ya kutaja idadi hiyo ya mashahidi, Mramba aliliambia jopo linaloongozwa
na Jaji John Utamwa akisaidiwa na Jaji Sam Rumanyika, Msajili Sauli
Kinemela kuwa shahidi wa sita ambaye wanatarajia kumwita, bado
hajathibitisha kama atakwenda kutoa ushahidi au la.
Mramba
alieleza kuwa kati ya mashahidi hao anaotarajia kuwaita kumtetea,
watatu watawasilisha nyaraka na wengine watafika mahakamani.
Licha ya kuwataja mashahidi hao, Mramba aliiambia Mahakama kuwa atatoa utetezi wake kwa njia ya kiapo.
Mbali
na Mramba, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu
Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja nao wameiambia Mahakama
kuwa na wenyewe watajitetea kwa njia ya kiapo na pia watatetewa na
mashahidi hao.
Lakini Mgonja aliongeza shahidi mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Karisti.
Baada
ya kutoa taarifa hiyo, Mramba alianza kujitetea na Wakili wake Hurbert
Nyange alimtaka aieleze Mahakama chimbuko la kesi inayomkabili.
Mramba
alisema ana umri wa miaka 71. Alidai kuwa chimbuko la kesi hiyo ni
malalamiko yaliyokuwapo bungeni kwa wananchi na kwenye vyombo vya habari
kuwa ingawa Tanzania ina migodi kadhaa ya dhahabu, haijafaidika kwa
sababu migodi hiyo ilikuwa inaiibia Serikali na kuidanganya juu ya
uzalishaji na uuzaji wa madini hayo nje ya nchi.
Alidai
kuwa kutokana na malalamiko hayo, Serikali ilibidi kuchukua hatua ya
kujibu hoja hizo zilizojitokeza katika jamii. Hivyo iliileta kampuni ya
Alex Stewart Government Business Assayers kukagua migodi hiyo ili
Serikali ipate maelezo juu ya malalamiko ya wananchi.
Mramba
aliendelea kueleza kuwa Serikali iliiteua BoT ifanye kazi ya kutafuta
kampuni inayoweza kufanya kazi hiyo kwa niaba yake na ikafanya hivyo kwa
kuingia mkataba na kampuni iliyochaguliwa ya Alex Stewart Government
Business Assayers.
“Kampuni
ya Alex Stewart Government Business Assayers ni kampuni ambayo ipo
katika kundi la kampuni za Alex Group ambazo makao makuu yake yapo
nchini Uingereza, lakini kampuni hiyo ya Alex Stewart Government
Business Assayers makao makuu yake yapo nchini Marekani,” alisema
Mramba.
Alidai
kuwa aliyeagiza BoT kufanya kazi hiyo ya kumtafuta mkaguzi wa dhahabu
ni Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na kwamba wakati huo yeye akiwa
Waziri wa Fedha alipewa jukumu la kuhakikisha gharama za kumlipa
mkaguzi huyo zinapatikana ndani ya Serikali, BoT au popote.
Alidai
kuwa kati yake na Gavana, hakuna aliyekuwa na mamlaka juu ya mwingine
na kwamba Gavana alikuwa na wajibu wa kufanya mchakato wa kumtafuta
mkaguzi wa dhahabu.
Mramba
alisisitiza kuwa yeye hakuhusika kwenye mchakato huo kwa kumtafuta wala
kumleta hapa nchini wala kumtuma mwakilishi yeyote kumwakilisha kwenye
kamati iliyoteuliwa kufanya mchakato huo, bali alipewa agizo la kumlipa.
“Mimi
kama waziri sikuwa na mtu wangu kwenye ile kamati lakini Wizara ilituma
mwakilishi, ambaye alikuwa Mwanasheria Bethar Soka wakati wa kuhoji
kampuni mbili ili wachague na kwenye kujadili vipengele vya mkataba,”
alisema Mramba wakati akitoa utetezi wake.
Mramba
alidai kuwa katika mchakato huo, Bethar aliwahi kuandika barua TRA
(Mamlaka ya Mapato Tanzania) akiomba ushauri juu ya kipengele kilichopo
kwenye mkataba huo kinachotoa msamaha wa kodi.
Baada
ya Mramba kueleza hayo, Nyange aliiomba Mahakama imruhusu kuzungumza na
mteja wake, Jaji Utamwa alimruhusu. Hata hivyo, mazungumzo yao yalikuwa
ya kunong’ona kitendo ambacho kilimfanya Wakili Mkuu wa Serikali,
Fredrick Manyanda kupinga akiomba wazungumze kwa sauti ili na wao
wasikie.
Manyanda
baada ya kutoa pingamizi hilo, Nyange alisema kwa sauti kuwa alikuwa
akimwambia mteja wake aache kuzungumza juu ya mambo aliyoyasikia na yale
asiyoyajua, bali azungumze kile ambacho anakifahamu.
Kutokana
na hoja hiyo, Mramba alidai kuwa wakati Bethar akiwa kwenye kamati
(timu) hiyo, yeye hakuwapo wala hakujua alichoagizwa na kwamba hakuwahi
kumpa mfanyakazi wake maagizo yoyote kwenye kamati hiyo na hajui Wizara
ya Fedha ilikuwa na mamlaka gani kwenye makubaliano.
Mramba
aliongeza kudai kuwa BoT katika kusimamia uchumi, ndiyo yenye wajibu
wa kumshauri Waziri wa Fedha, lakini Waziri wa Fedha hawezi kuishauri
BoT au Gavana.
Alibainisha
kuwa mkataba kati ya Kampuni ya Alex Stewart Government Business
Assayers na Serikali, ulisainiwa na aliyekuwa Gavana wa BoT, hayati
Daud Balali na Makamu wa Rais wa kampuni hiyo, Erwine Frorence.
Alidai kuwa Gavana alisaini kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo pamoja na agizo la Rais.
Akimhoji Mramba Wakili Nyange alisema: “Inasemekana kama isingekuwa wewe Gavana asingesaini huo mkataba.”
Mramba alijibu: “Mimi sikumwambia Gavana asaini, nilimwambia afungue mkataba na siyo asaini mkataba.”
Mramba
alidai kuwa tangu mwanzo, Gavana mwenyewe aliomba asaini, lakini yeye
na Waziri wa Nishati na Madini baada ya kujadili na kukubaliana,
walimtaka afungue mkataba ili baadhi ya vitu fulani vianze
kushughulikiwa ili hatimaye asaini na utekelezwe... “Nilimwambia don’t
sign (usisaini) nikampa na sababu.”
Jaji Utamwa ameiahirisha kesi hiyo hadi leo saa 7:00 mchana Mramba atakapoendelea kutoa utetezi wake.
Mramba,
Yona na Mgonja walifikishwa mahakamani mwaka 2008. Inadaiwa kuwa, kati
ya Agosti, 2002 na Juni 14, 2004, Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa
watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia
Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao waliipatia msamaha wa kodi isivyo halali, Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.