SERIKALI
imesema eneo linalogombewa na Malawi katika Ziwa Nyasa ni mali ya
Tanzania na sasa imeziamuru kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa
mafuta kuondoka eneo hilo kuanzia jana.
Onyo
hilo dhidi ya Malawi lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia amesisitiza kuwa
Tanzania itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho
la kiusalama.
Hii
ni mara ya pili Serikali kuionya Malawi katika mgogoro huo. Wiki
iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni
Samuel Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi.”
Sitta
alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki,
Godfrey Zambi aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana,
akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka
2012/13, bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika
ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema
pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku
ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua
katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali
ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na
shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo
(jana),” alisema Membe.Alisema Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda
mipaka yake kwa gharama yoyote na haitaruhusu utafiti huo wa uchimbaji
wa gesi na mafuta uendelee.
Alisema
chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania
watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la
kiusalama.
Kiini cha Mgogoro
Kuhusu
kiini cha mgogoro, Waziri Membe huku akirejea historia ya mipaka tangu
ukoloni, alisema ni hatua ya Serikali ya Malawi kushikilia msimamo kuwa
eneo lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi wakati Tanzania inashikilia kuwa
mpaka upo katikati ya Ziwa.
“Wenzetu
wanadai ziwa lote lipo Malawi lakini, nyaraka zilizotengenezwa na
wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa
hilo upo katikati,” alisema. Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu
kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo kama hilo linafanana na
mgogoro uliokuwepo baina ya Cameroon na Nigeria.
0 comments:
Post a Comment