Kitengo cha Utafiti wa Dawa Asilia cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kimegundua dawa za asilia za aina tatu za kutibu magonjwa ya kisukari na kibofu cha mkojo.
Kitengo hicho ambacho kazi yake ni utafiti
wa dawa asilia, kimefanikiwa kugundua dawa hizo katika kipindi cha
miaka 38 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974.
Dawa zilizogundulika na kuonyesha
mafanikio makubwa ni aina ya Morizela zilizopo kwenye mfumo wa juisi
ambazo moja ina sukari na nyingine haina ambazo zimeonyesha mafanikio
makubwa katika tiba ya kisukari.
Dawa nyingine ni aina ya Prucan ambayo
hutibu wagonjwa wenye matatizo ya kutopata haja ndogo, magonjwa ambayo
huwapata zaidi wanaume wazee.
Akizungumza na gazeti hili, Kaimu
Mkurugenzi wa kitengo hicho, Dk. Ester Innocent, alisema pamoja na
kwamba dawa hizo zimeshaanza kutumika, lakini bado hazijaingia sokoni
kwa vile bado ziko kwenye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Alisema TFDA ikishatoa usajili wake,
kitengo hicho kinaweza kuingia mikataba na wenye kampuni za kutengeneza
dawa ili zizalishwe kwa wingi na kuwafikia wagonjwa wengi popote walipo.
Alisema kwa sasa dawa hizo zinapatikana
kwa uchache sana kutokana na kuzalishwa hospitalini hapo na ikishapata
usajili, itapatikana kwa wingi.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi huyo,
pamoja na kitengo hicho kuanza muda mrefu na hatimaye mwaka huu kutoa
rasmi dawa hizo, wengi wataona imechukuwa muda mrefu lakini akasisitiza
kuwa utafiti kwa kawaida huchukuwa muda mrefu.
Dk. Innocent alisema watafiti mara nyingi
ni wepesi kugundua tiba ya dawa, lakini dawa hiyo haiwezekani kutumika
bila kujua madhara yake, hivyo wanalazimika kuanza tena utafiti wa
kuyajua madhara hayo na kuyadhibiti.
Hata hivyo alisema zipo dawa nyingi za
asili zinazofanyiwa utafiti lakini ambazo utafiti wake uko karibuni
kukamilika ni za aina 11 zinazotibu magonjwa mbalimbali kama malaria,
pumu, tumbo, ngozi na magonjwa nyemelezi ya ukimwi.
Alisema kitengo hicho kinakabiliwa na
changamoto nyingi hasa za uhaba wa fedha na hivyo kujikuta kuchelewa
kutoa matokeo ya tafiti zao kwa wakati.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment