ZITTO ASEMA YUMO KIONGOZI WA JUU WA SERIKALI YA SASA,WENGINE NI WA AWAMU YA MKAPA, ATISHIA KUWAANIKA
TUHUMA
kwamba baadhi ya vigogo Serikali wameficha mabilioni ya fedha nchini
Uswisi jana ziliibuka tena bungeni, huku Kambi ya Upinzani ikidai kwamba
inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali
haitawataja.
Naibu
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe aliitaka Serikali kuwataja
kwa majina viongozi na wafanyabiashara wakubwa walioficha Sh315.5
bilioni nchini Uswisi, akisema kwamba watu hao “wanafahamika”.
Juni
mwaka huu, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa inayoonyesha kuwapo kwa
kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini
humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Akiwasilisha
hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na
Uchumi bungeni jana, Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo
alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa
Serikali za awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo.
“Kambi
ya Upinzani bungeni imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu
kabisa wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni
mwa fedha hizi,” alisema Zitto.
Pia
aliitaka Serikali kuliambia taifa ni hatua gani itakazochukua kurejesha
fedha hizo pia kuwataka wamiliki wake na kama ikishindwa, wao
watawataja.
“Tunaitaka
Serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya
taarifa ile kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa,” alisema Zitto
na kuongeza:
“Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya
watu wenye umiliki wa fedha hizo iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi,”
alisisitiza.
Fedha
hizo zinadaiwa kutokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji
wa Serikali na wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na
kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na
gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka
2004 na 2006.
Baada
ya Zitto kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro (CCM),
Christopher Ole-Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo.
Sendeka
alisema Zitto alisema miongoni mwa walioficha fedha hizo ni kiongozi wa
juu wa Tanzania, lakini akashangaa Serikali kutohoji juu ya kauli hiyo.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, mheshimiwa Zitto amewatuhumu viongozi wa Serikali na
kiongozi wa juu kabisa kuwa wameficha fedha Uswisi,” alisema.
Alisema,
lakini pamoja na tuhuma hizo, hakuna kiongozi wa Serikali aliyesimama
na kutolea ufafanuzi hivyo akaomba mwongozi ili Zitto aruhusiwe
kuwataja.
Sendeka
alisema tuhuma hizo ni nzito na zimeichafua sura ya Serikali hivyo ni
vyema ijulikane ni nani kati ya Serikali na Zitto atabeba mzigo wa
kuwataja.
Naibu
Spika, Job Ndugai alisema angetoa mwongozo huo baada ya kuipitia hotuba
hiyo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuona kama ina matatizo.
Hata hivyo, hakutoa mwongozo huo.
Chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment