Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana (Zebras)
katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka
huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole
ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa
zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika
ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki
Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari
mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na
Lemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa
Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi
Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji
alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya
kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki Aggrey
Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi
zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd. Safari hii Zebras
ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi
aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na
mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto
Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea rafu
mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia
Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon
Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya
ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha
washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi
kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti
washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi
yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye
timu kwa mara ya kwanza. Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia,
hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada ya
mechi hiyo.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi,
Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano,
Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick
Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo
Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani
kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya
Airways.
0 comments:
Post a Comment