Wednesday, August 15, 2012

Dk. Slaa afanyiwa ‘umafya’

Meneja wa hoteli amnyang`anya chumba

 Umeme wakatika, Tanesco wakana hujuma

 
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amefukuzwa katika nyumba ya kulala wageni ndani ya Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kisiasa ikiambatana na kuzimwa kwa umeme kwa mji mzima kwa saa zaidi ya 12 ili kudhibiti mikutano yake ya hadhara anayoifanya.

Dk. Slaa ambaye aliwasili majira ya saa 8.00 mchana mjini Mikumi akitokea tarafa ya Malinyi, wilayani Ulanga, Morogoro, katika Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni Sangara, alifikwa na udhalilishaji huo baada kuonyeshwa chumba chake lakini baadaye akanyang’anywa.

Baada ya kuwasili hotelini hapo, Dk. Slaa alikabidhiwa funguo ya sehemu ya kufikia kutoka kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, na kuingia chumbani, muda mfupi baada ya kuingia katika chumba hicho alitokea meneja wa hoteli hiyo, Jacob Sumary, na kumueleza kuwa sehemu hiyo imeshawekewa ‘oda’ na wateja wengine na hivyo kutakiwa kuondoka katika eneo hilo mara moja.

Hata hivyo, Dk. Slaa alihoji sababu za mmoja wa walimu wa Veta kuacha majukumu yake na kujipa jukumu la kuhudumia hoteli kwa kumhudumia eneo lenye vyumba vitatu lenye thamani ya Sh. 75,000 kwa kila chumba kimoja Sh. 25,000.

Meneja huyo alishikilia kumtaka Dk. Slaa aondeke hotelini hapo kwa kuwa yeye hakuwa na taarifa za ujio wake. Dk. Slaa alitii na kuondoka.

Naye Sumary alipofuatwa na NIPASHE jana kwenye hoteli hiyo kuzungumzia kitendo cha kumnyang’anya Dk. Slaa malazi, alikataa kuzngumzia suala hilo.

Awali alisikiliza NIPASHE ikimuuliza juu ya hatua alizochukua na kutaka kujua ni kwa nini, lakini alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na kukata simu yake.

Akizungumzia hali hiyo katika mkutano wa hadhara, Dk. Slaa alisema kuna mipango imefanywa kwa nia ya kumdhoofisha katika kampeni za kuwakomboa Watanzania.

“Kama mimi nafanyiwa mambo hayo kwa suala dogo la malazi tu na serikali ya CCM, je nyinyi wengine mtafanyiwaje? Mnapaswa kujifikiria mara mbili,” alisema Dk. Slaa.

Ghafla umeme ulizimwa katika mji wa Mikumi hali iliyotafsiriwa kuwa ni muendelezo wa hujuma zinazofanywa dhidi ya Chadema, kwani wananchi walidai mji huo haukuwa na tatizo la umeme.

“Watanzania wa leo siyo wa jana. Zimeni umeme. Hata mfanye nini tutaendelea na mkutano na wananchi watatusikiliza tu. Lakini nitakula nao sahani moja waliofanya hivi,” alisema Dk. Slaa.

Hata hivyo, kukatika kwa umeme huo kuliongeza mori kwa wakazi wa Mikumi kutokana na kuongezeka kwa wingi katika mkutano huo na kukemea vitendo vilivyofanywa na serikali dhidi ya Dk. Slaa.

Akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Morogoro, Deogratius Ndamugaba, alisema kukatika kwa umeme kulitokana na hitilafu za kawaida na siyo hujuma au msukumo wa kisiasa.

“Kukatika kwa umeme Mikumi siyo kwa sababu ya Chadema ila ni feeder ya Mikumi iko nje tangu saa 12.45 jioni. Nguzo imeanguka na inapaswa kubadilishwa na sehemu yenyewe ni porini. Kuna giza na Chui,” alisema Ndamugaba.

Alisema amekuwa akijaribu kuwasiliana na vyombo vya habari ili kuwapa taarifa wananchi wa Mikumi.

Alisema utendaji kazi wa eneo hilo kwa muda huo ulionekana kuwa mgumu na kwamba, tayari mafundi wa Tanesco walikuwa katika eneo la tukio kufanya marekebisho.

chanzo: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment