Wednesday, August 15, 2012

TFF yamkataa Twite Simba, Yanga


 

Na Wilbert Molandi
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema halitambui usajili wa beki wa kati wa kimataifa wa Rwanda na APR, Mbuyu Twite (pichani).
Klabu kongwe za Yanga na Simba, hivi sasa zipo kwenye vita kali zikimgombea beki huyo ambaye awali ilidaiwa alisaini Simba kwa dola 30,000 (zaidi ya Sh milioni 45), kisha akapewa dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 75) na kusaini Yanga.
 Vita hiyo hivi sasa imeingia katika sura nyingine baada ya Simba kumwekea mawindo makali beki huyo ikiwemo kutishia kumshitaki kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema hadi hivi sasa hawajapokea jina la beki huyo kutoka kwa Simba wala Yanga.
Osiah alisema majina ya usajili waliyoyapokea hadi sasa ni ya Azam FC na Kagera Sugar pekee, hivyo wanashangaa wao TFF kuingizwa kwenye vita hiyo, wakidaiwa wanaihujumu Simba.
Alisema ili usajili ukamilike, lazima TFF ipate orodha ya wachezaji ambao klabu zimewasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Ujue sisi tunashindwa kuelewa TFF tunaingizwa vipi katika suala la usajili wa Twite, kazi yetu ni kupokea orodha ya wachezaji ambao klabu imewasajili katika kipindi husika.
“Kama TFF tunasema hatutambui usajili wa Twite, hatujapokea jina lake kutoka kwenye klabu hizo zinazomgombea (Simba na Yanga), timu zilizowasilisha majina ya wachezaji wao ni Azam FC na Kagera Sugar tu,” alisema Osiah.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mashindano ya TFF, Saad Kawemba, amezitaka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara kuwa makini katika suala la usajili.
“Nawakumbusha viongozi wa klabu za ligi kufuata maelekezo ya usajili tuliyowapa katika kozi maalum ya kutumia TMS (mtandao wa usajili).
“Klabu inatakiwa kufanya mazungumzo na timu inayommiliki mchezaji, njia hiyo inasaidia kupata ukweli wa mkataba wake,” alisema Kawemba.

0 comments:

Post a Comment