Na. Aron Msigwa -MAELEZO.
Zikiwa
zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na
makazi nchini, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki ametoa
wito kwa wakazi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa
watakaoendesha zoezi hilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam amesema maandalizi ya
ukamilishaji wa zoezi hilo yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa Waziri
mkuu Mizengo Pinda anatarajia kuzindua kampeni ya uhamasishaji wa watu
kushiriki katika zoezi hilo kesho (17/8/2012) katika viwanja vya Mnazi
Mmoja jijini Dar es salaam.
Ametoa
onyo na kuvitaka vikundi vya baadhi ya viongozi wa dini na wananchi
wanaowahamasisha wananchi kutoshiriki katika zoezi hilo katika maeneo
yao kuacha mara moja kwani zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria namba 1
ya mwaka 2002.
"Natoa
onyo kwa kikundi chochote kinachoendesha kampeni ya kuwahamasisha
wananchi kutoshiriki kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi katika mkoa
wa Dar es salaam kuacha mara moja kwani zoezi hilo lipo kwa mujibu wa
sheria na yeyote atakayekaidi au kukwamisha zoezi hilo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake" amesema.
Amesema
kuwa Zoezi la Sensa sio la mtu mmoja mmoja wala kikundi fulani bali ni
suala la watanzania wote bila kujali dini, rangi wala kabila, hivyo watu
wanaopinga zoezi hilo wanavunja sheria za nchi.
Naye
mratibu wa zoezi la Sensa kwa mkoa wa Dar es salaam Bi. Magreth
Stephen Mganda amesema mpaka sasa mkoa wa una jumla ya makarani na
wasimamizi 18,993 watakaoshiriki zoezi la kuhesabu watu wakiwemo 90 wa
akiba.
Amesema kati ya hao 644 wanatoka wilaya ya Kinondoni,365 wanatoka Ilala na 530 kutoka wilaya ya Temeke.
Katika
hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki
ametoa ufafanuzi wa vitendo vya vurugu,uharibifu na uporaji wa mali za
wanachi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es salaam hususan
wilaya ya Temeke na Kinondoni.
Amesema
kuwa vitendo hivyo vilivyotokea ni kinyume cha sheria na kutoa onyo
kwa wale wote waliohusika kuvamia maeneo na kuchukua ardhi kwa nguvu
pasipo kufuata utaratibu kuacha mara moja.
Amesema
kuwa wale waliovamia maeneo hayo bila kufuata utaratibu waondoke
wenyewe na kukubali kutii sheria bila shuruti kwa kuwa serikali
haitamvumilia mtu yeyote anayevunja sheria.
"Wale
wote waliovamia maeneo hayo katika mkoa wa Dar es salaam katika maeneo
yote yenye vurugu waondoke wenyewe , watii sheria kwa sababu vitendo vya
namna hii ni vya kiharifu na kamwe serikali haiwezi kuvivumilia"
amesisitiza.
Ameongeza
kuwa tayari mahakama imeshatoa mwongozo kuhusu maeneo hayo na
kubainisha kuwa wote waliohusika na watakaoendelea kuvunja sheria katika
maeneo hayo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
0 comments:
Post a Comment