TUHUMA
za rushwa dhidi ya wabunge juzi zilitawala kikao cha Kamati ya Wabunge
wa CCM, ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliombwa kuingilia kati ili
‘kuwasafisha’ wenye tuhuma hizo mbele ya jamii. Kikao hicho kiliitishwa
pamoja na mambo mengine, kuzungumzia nafasi ya wabunge wa CCM katika
kuhamasisha umma kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika
Agosti 26, mwaka huu na utoaji wa maoni kwa Tume ya Katiba Mpya.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho, zimesema pamoja na kwamba haikuwa moja ya
agenda za mkutano huo, Mbunge wa Bukene, Seleman Zedi alisimama na
kuibua kilio cha wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa. Mbunge huyo ambaye
pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na
Spika wa Bunge, Anne Makinda alimweleza Waziri Mkuu kwamba baadhi ya
wabunge, hasa wa iliyokuwa kamati yake, wangekwendaje kuhamasisha Sensa
majimboni wakati wamechafuka kwa tuhuma za rushwa?
Mtoa
taarifa wetu anasema, mbunge huyo akiungwa mkono na Mbunge wa Viti
Maalumu, Munde Tambwe, walimwomba Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti
wa kikao hicho, amweleze Spika awasafishe kwa kutangaza bungeni kwa madai kuwa tuhuma dhidi yao hazikuthibitika.
Alisema
kauli hiyo ya Spika ingewasaidia kurudi majimboni wakiwa wasafi na
wenye mamlaka ya kimaadili kuungana na wenzao kuhamasisha Sensa na
utoaji wa maoni ya Katiba Mpya. Hata hivyo, vyanzo vyetu vya habari
vimetofautiana kuhusu kauli ya Pinda baada ya kupokea malalamiko hayo,
kimoja kikisema alikaa kimya na kingine kikisema alijibu kuwa
asingeweza kuingilia kati suala hilo kwa kuwa bado linachunguzwa na
Kamati ndogo ya Bunge. Mambo mengine yaliyoibuka kwenye kikao hicho ni
mjadala wa Muswada wa Fedha.
Wabunge
wa CCM walipinga ongezeko la kodi kwenye maji ya kunywa na msamaha wa
Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa kampuni za kuchimba madini. Kwa
zaidi ya wiki sasa, Kamati ndogo ya Bunge iliyoundwa na Spika Makinda
imekuwa inaendelea kuwahoji baadhi ya wabunge ama wanaotuhumiwa au
wenye ushahidi wa tuhuma hizo. Baadhi ya wabunge wamekuwa wakiitwa mmoja
baada ya mwingine na kuhojiwa na wajumbe hao faragha kuhusu ama madai
ya rushwa dhidi yao au mambo waliyoeleza kuhusu tuhuma hizo. Tuhuma hizo
zilisababisha Spika Makinda kuvunja Kamati ya Nishati na Madini
iliyodaiwa kukithiri kwa rushwa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment