Tarehe
16 Agosti, 2012 gazeti la Rai Toleo Na.986 katika ukurasa wake wa
kwanza na watatu lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari “UCHIMBAJI
WA URANI SERIKALI YAONYWA” na kuwa kumezuka sakata lingine ambapo
kampuni ya kigeni imeanza kuchimba madini hatari aina ya urani kwa kile
wachunguzi wanasema ni kinyume cha sheria.
Gazeti
hilo liliendelea kuandika kwamba Tanzania haina sera ya urani na
kwamba hata kama Serikali imeruhusu uchimbaji huo, ni kinyume cha sheria
kwa sababu hata Serikali yenyewe haijatunga sheria ya uchimbaji urani.
Tunasema habari hii ina malengo ya kuupotosha umma.Mwandishi wa habari
hii bila ya kutaja jina lake anaeleza kuwa hakuweza kuwasiliana na
viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini licha ya yeye kuwaandikia ujumbe
kitu ambacho hakina ukweli. Kutokana na unyeti wa habari yenyewe
mwandishi alipaswa kuhakikisha anapata taarifa kamili kutoka Wizarani na
siyo kutoa taarifa kwa matakwa binafsi.Habari hii imelenga zaidi katika
kuupotosha umma badala ya kuuelimisha kama ambavyo mwandishi ameshindwa
kueleza kwa ufasaha ni nini hasa kusudio lake.
Tunaheshimu
Uhuru wa vyombo vya Habari na tungependa kama kuna suala lolote
linalohitaji ufafanuzi, Wizara ipo tayari muda wowote kutoa maelezo
badala ya kukimbilia kuandika habari zinazojichanganya na kusababisha
usumbufu kwa wananchi.
Tunatumia
fursa hii kwa mara nyingine kuufahamisha umma kuwa kama Mheshimiwa
Waziri wa Nishati na Madini Mhe: Prof Sospeter Muhongo alivyosema kwenye
hotuba ya bajeti ya mwaka huu kuwa pamoja na kuwepo kwa maeneo
mbalimbali hapa nchini yenye madini ya urani ni maeneo mawili yaani
Wilaya ya Namtumbo na Manyoni ndiyo yaliyothibitishwa kuwa na kiasi cha
kutosha kuweza kuchimbwa kibiashara na si kweli kuwa uchimbaji umeanza.
Eneo
la Namtumbo lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa na Serikali iliwasilisha
maombi UNESCO ya kurekebisha mipaka ya eneo la hifadhi ya Dunia ili
kuongeza eneo la mradi, ombi liliridhiwa katika kikao cha UNESCO cha
tarehe 02/Julai, 2012 kilichofanyika Saint Petersburg (Urusi).Aidha,
Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Kanuni za Madini ya Mionzi Ayonisha za
Mwaka 2010 - the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 chini
ya Sheria ya Madini, 2010 zinatumika katika kusimamia shughuli za
utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani nchini.
Sheria
na Kanuni zote zilizotungwa na zitakazoendelea kutungwa zinazohusiana
na usimamizi wa madini ya urani pamoja na mambo mengine zinalenga
kuzingatia miongozo/taratibu za Shirika la Kimataifa la Nguvu za
Atomiki (IAEA) za usimamizi wa madini hayo zinazohakikisha kuwa
uchimbaji hauleti athari kwa binadamu na mazingira.Tunaendelea
kuwashauri waandishi wa habari kuwa sisi kama wizara na chombo cha
Serikali tunawajibu wa kuelimisha umma juu ya shughuli mbalimbali za
wizara hivyo tunawashauri kuwa tushirikiane kwa maslahi ya Taifa badala
ya kutoa habari zenye malengo binafsi.
Imetolewa na:Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini
0 comments:
Post a Comment