Thursday, August 16, 2012

Majambazi wapora Sh. milioni 65 Dar

 
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela
Watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi wamepora Sh. milioni 65 kwenye kiwanda cha kutengeneza kinywaji cha Sayona, kilichopo eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 machana baada ya majambazi hao kufyatua  risasi mara tatu hewani mfululizo kwa wakiwa wamesimama mbele gari la kiwanda  kiwanda hicho lililokuwa likitoka nje kupeleka pesa hizo kwa mhasibu wa kampuni ya M.M inayoshughulika na utengenezaji wa vifaa vya ujenzi.
Meneja masoko wa kampuni hiyo, Ragu Gadabi, alisema walinzi wake walimfungulia geti na kutoka nje ili kuwahisha pesa hizo. Alisema kuwa hatua chache nje ya geti, gari lenye  namba T640 MBZ aina ya RAV4 lilisimama mbele yake na kisha mtu mmoja alishuka na kugonga dirisha la gari lake.
“Sikuweza kufungua dirisha, lakini nilisikia milio ya risasi ikishambulia gari hilo, nilifanikiwa kutoka kwenye gari na kurudi kiwandani, lakini pesa na Laptop zote zimechukuliwa,” alisema na kuongeza: “Nilirudi kiwandani haraka kunusuru maisha yangu la sivyo wangepoteza uhai wangu, kitendo kilikuwa cha haraka mno yaani kufumba na kufumbua,” alisema Ragu.
Shuhuda ambaye hakupenda kutaja jina lake liandikwe gazetini, alisema majambazi hao walitokea barabara ya ITV na mara walipofika karibu na kiwanda hicho walisimama. Alisema muda mfupi baadaye aliliona gari likitoka kiwandani na kisha gari lililokuwa limesimama likalikinga gari hilo na kuanza kufyatua risasi na kufanikiwa kuchukua pesa na kompyuta ndogo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa Jeshi la Polisi linaedelea kulifanyia kazi.
“Nimepata taarifa hizo, lakini kwa sasa nipo nyumbani kwani hali yangu siyo nzuri kiafya, lakini vijana wangu wa kazi wanaedelea kuifanyakazi hiyo,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment